Sunday, March 4, 2012

WANAFUNZI WALEMAVU WAPIMWE KIUPEKEE - WALIMU!

Baadhi ya wanafunzi wa darasa la nne (viziwi) katika Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru wakiandika darasani.
Mmoja wa wanafunzi wenye ulemavu (kiziwi), Shule ya Msingi Iliboru akiandika darasani kama alivyokutwa na mpiga picha wa Thehabari.
Mwalimu Mkuu wa Kituo cha Wanafunzi wenye Ulemavu, Shule ya Msingi Naurei wilayani Arumeru, Tuzie Mtenga akizungumza na mtandao.

Baadhi ya walimu waliopo katika mafunzo ya vitendo katika Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru wakifundisha darasa la walemavu.

Na Joachim Mushi, Thehabari.com-Arumeru

BAADHI ya walimu wa wanafunzi wenye ulemavu anuai wilayani hapa wameitaka Serikali kuacha utaratibu wa kuwataini wanafunzi wenye ulemavu katika mitihani ya taifa kwa vigezo sawa hasa upande wa muda wa kufanya mitihani husika.
Wamesema hali hiyo inawanyima baadhi ya wanafunzi wenyeulemavu kujipima kiusahihi kutokana na dosari zao na wanafunzi wa kawaida hivyo kujikuta wengi wakifanya vibaya au kutopata daraja stahili kwenye matokeo.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini hapa, Mwalimu Mkuu wa Kituo cha Wanafunzi wenye ulemavu, Shule ya Msingi Naurei wilayani Arumeru, Tuzie Mtenga amesema kitendo cha kuwachanganya wanafunzi hao baadhi yao wameishia kufanya vibaya katika masomo yao hasa kwenye mitiani ya mwisho kitaifa.
“Mwanafunzi mwenye ulemavu baada ya kumaliza mafunzo kwenye vitengo vyao tumekuwa tukiwachanganya kwenye madarasa ya kawaida shule za msingi, wanaendelea na baadaye wanafanya mitihani ya taifa kwa muda sawa na wengine hiki si kipimo sahihi kwa kweli,” alisema Mtenga ambaye kituo chake kinawalemavu wa akili na viungo.


Naye mwalimu, Rams Mosha wa Chuo cha Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu Usa River amesema wapo wanafunzi wenye ulemavu ambao kasi yao ya uandishi ni tofauti na mwanafunzi wa kawaida na wanauelewa lakini wamekuwa hawapati haki pale wanapotahiniwa kwa vigezo sawa hasa muda na wanafunzi wengine.
“Walemavu wengine wanaandika huku wakitetemeka sasa mtu kama huyu waweza kukuta anafanya vizuri darasani lakini kwa kuwa baadaye anafanya mtihani wa taifa kwa muda sawa na watahiniwa wa kawaida anaweza asimalize mtihani au kutofanya vizuri…hili aliangaliwi na mamlaka husika,” alisema Mosha ambaye naye ni mlemavu wa viungo.


Kwa upande wake Mwalimu Mratibu wa Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru, Loitusho Yamat ipo haja ya wanafunzi walemavu kufuatiliwa kwa karibu tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wameshindwa kufanya vizuri kutokana na usimamizi afifu uliopo kielimu.
Yamat ambaye shule yake ina jumla ya wanafunzi walemavu 60, yaani wanafunzi viziwi na wale wenye mtindio wa ubongo alisema kwa sasa kituo hicho kimetafuta ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa shule ndogo ya sekondari kwa wanafunzi wenye ulemavu ili kuwafuatilia kwa karibu baada ya masomo ya msingi.
Habari na picha zote zimeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com kwa ushirikiano na Kituo cha Habari Kuhusu Ulemavu Tanzania (ICD).

No comments:

Post a Comment