Thursday, March 8, 2012

MGOGORO WA NDANDA SEKONDARI WAMALIZIKA, SERIKALI NA VIONGOZI WA TAASISI ZA KIISLAMU WAKUBALIANA KUWARUDISHA WANAFUNZI 62 WALIOFUKUZWA!

Naibu Katibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bw. Selestine Gesimba (katikati) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu makubaliano baina ya Serikali na Viongozi wa Taasisi za Kiislamu kuhusu mgogoro wa shule ya Sekondari Ndanda iliyoko Masasi mkoa wa Mtwara leo jijini Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine serikali itawarudisha shuleni mwaka huu wanafunzi wote 62 waliohusika na mgogoro wa shule hiyo. Wengine kutoka kushoto ni Sheikh Musa Kundecha, Amir wa Baraza kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania na Bw. Samweli Kusaga kutoka Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi, Idara ya Sekondari.

Viongozi wa Taasisi za Kiislamu Tanzania wakiongozwa na Sheikh Musa Kundecha (pili kutoka kulia) ambaye ni Amir wa Baraza kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania wakijadili jambo na Rais wa Jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu Tanzania (TAMSYA) Jaafar Mneke (katikati) leo jijini Dar es salaam mara baada ya kumalizika kwa mkutano uliojadili makubaliano baina ya Serikali na Viongozi wa Taasisi za kiislamu kuhusu mgogoro wa shule ya sekondari Ndanda.
Rais wa Jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu Tanzania (TAMSYA) Jaafar Mneke (kulia) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ya kusitishwa kwa maandano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kesho nchini nzima kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kuhusu mgogoro wa shule ya sekondari Ndanda.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Ndanda waliosimamishwa masomo kufuatia mgogoro wa shule hiyo wakifuatilia tamko la makubaliano ya viongozi wa dini ya kiislamu na Serikali lililotolewa leo jijini Dar es salaam na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bw. Selestine Gesimba kufuatia mkutano wa pamoja uliofanyika tarehe 7 mwezi huu.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Ndanda waliosimamishwa masomo yao kufuatia vurugu zilizotokea katika shule hiyo wakitoka ndani ya jengo la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kusoma makubaliano uliowahusisha viongozi wa dini ya Kiislamu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na waandishi wa habari ambapo makubaliano hayo yameeleza kuwa serikali itawarudisha shuleni wanafunzi wote 62 waliosimamishwa, kuhakikisha kuwa shule ya sekondari Ndanda ina mazingira mazuri kwa wanafunzi wa dini zote kitaaluma na kuwawezesha kufanya ibada zao, shule zote zilizotaifishwa ni miliki ya serikali kiuendeshaji, ardhi na majengo vyote ni mali ya serikali na serikali kufanya utaratibu wa kuwepo vikao na viongozi wa asasi za dini zote.    Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.

No comments:

Post a Comment