Thursday, February 16, 2012

ZITTO KUONGOZA ZIARA YA CHADEMA KUKAGUA UHAI WA CHAMA MKOANI TANGA!

                                                             TAARIFA KWA UMMA

Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), inapenda kuutarifu umma kuwa viongozi kadhaa wa kitaifa, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Mheshimiwa Kabwe Zitto watafanya ziara ya kichama mkoani Tanga.

Ziara hiyo itakayoanza Jumamosi, Februari 18, 2012, itaanzia Wilaya ya Handeni, Korogwe, Mheza, Pangani, kisha Tanga Mjini. Katika maeneo yote hayo Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Zitto atakagua uhai wa chama mkoani humo, ambapo atafanya mikutano na wanachama wa CHADEMA.


Viongozi hao wa CHADEMA pia watazungumza na wananchi mkoani Tanga katika mikutano ya hadhara, kwenye maeneo yote hayo. Watatumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa na yale ya maeneo husika.

Mbali ya kukagua uhai wa chama mkoani Tanga, katika ziara hiyo, Mheshimiwa Zitto , pia atatumia fursa hiyo kuipeleka kwa wananchi na kuifafanua hoja yake aliyoiwasilisha bungeni katika mkutano ulioisha hivi karibuni juu ya zao za mkonge, ambapo baadhi ya wabunge wa Tanga, walisimama kuipinga hoja hiyo.

Kurugenzi ya Habari na Uenezi, inatoa wito katika maeneo yote ambayo msafara huo wa CHADEMA utafanya mikutano, wananchi wahudhurie kwa wingi ili wanufaike na ziara hiyo.

Imetolewa leo Februari 16, 2012, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Afisa Habari wa CHADEMA.

No comments:

Post a Comment