Monday, February 20, 2012

MAHAKAMA YA RUFAA YATUPILIA MBALI OMBI LA TANESCO KUKWEPA KUILIPA DOWANS BILIONI 94!

Mahakama ya Rufaa Tanzania imetupilia mbali ombi lililowasilishwa na Shirika la Umeme nchini Tanesco kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoamuru shirika hilo kuilipa Dowans zaidi ya shilingi Bilioni 94 kama ilivyoainishwa na Mahakama ya Kimataifa ya Biashara (ICC).

Katika maombi yake Tanesco iliwasilisha rufaa kwenye mahakama hiyo kuepukana na malipo hayo, lakini Dowans nayo ikaendelea kuibana kwa kuliwekea pingamizi shirika hilo ili linyimwe kibali hicho.

Akisoma hukumu yake, Jaji wa Mahakama hiyo Dk. Fauz Twaib amesema ombi hilo limekataliwa na kuziamuru pande zote kila moja kujilipia gharama za kesi hiyo na Tanesco imetakiwa kurudi mahakamani hapo Aprili 18 mwaka huu ili kuwasilisha ombi la kuzuia malipo hayo yasifanyike.

Septemba 28 mwaka jana, Jaji EMILIAN MUSHI wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, aliamua tuzo ya Dowans iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), isajiliwe ili kuwa hukumu halali ya mahakama hiyo.


Kwa uamuzi huo, Tanesco sasa inatakiwa iilipe Dowans Sh 111 bilioni badala ya shilingi Bilioni 94 za awali.

No comments:

Post a Comment