Sunday, January 22, 2012

MAIGE ATAKA VIGOGO WALIOVAMIA MISITU WATOLEWE!

Na Tulizo Kilaga, Ruvu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Ezekiel Maige, amewaagiza watendaji wa misiti kuhakikisha wanafanya zoezi la kitaifa la kuhakiki mipaka ya misitu nchini na kuwatoa wavamizi wote waliopo ndani ya hifadhi za misitu.


Mhe. Maige aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa katika ziara ya kutembelea Msitu wa Hifadhi wa Ruvu Kaskazini uliopo Kibaha, mkoani Pwani baada ya kuelezwa kuwa kuna baadhi ya vigogo wameuziwa na wanakijiji maeneo makubwa yaliopo ndani ya hifadhi kwa kujua ama kutokujua na kuweka mawe ya ardhi hali inayowawia vigumu kuwatoa. Kufuatia taarifa hiyo, Mhe. Maige aliwaagiza watendaji wake kuhakikisha wanashirikiana na wataalamu wa ramani kutoka Wizara ya Ardhi kuhakiki mipaka ya misitu na kuwabomolea wale wote walioko ndani ya mipaka ya hifadhi.


“Hakikini mipaka yenu na baada ya kubainisha mipaka hiyo, kama ambavyo tunavyofanya kule kwingine, kitakachofuata kwa wale walioko ndani ya hifadhi, kuna ile mikasi mwekundu, bomoa, wabomolewe haraka iwezekanavyo na hapo ndipo tutakapowabaini wazito ama wanene waliovamia hifadhi,” alisema Mhe. Maige.
Aidha, aliongeza kuwa ni lazima hatua zichukuliwe kwa kufanya uchunguzi kwani kuna maeneo ambayo wataalamu wa misitu waliopewa dhamana ya kuyalinda kwa makusudi wanajidahi hawajui mipaka na kuruhusu ardhi imegwe.

“Kuna matukio mawili matatu ambayo afisa misitu ameandikiwa na afisa ardhi, tunataka kutoa eneo hili kwa muwekezaji fulani, tunaomba utuhakikishie mipaka ya hifadhi kwamba haifiki kwenye eneo hilo, akaandika nakuhakikishia eneo hilo liko nje kwa sababu tu ameshawishiwa kwa namna ambayo ni vigumu mimi na wewe kujua,” “Sasa nitakapobaini watu wa namna hiyo ama kwa makusudi ama kwa bahati mbaya wameridhia shughuli za uendelezaji ama utoaji wa hati ifanywe, hao nitashughulika nao,” alisema Mhe. Maige.
Aliongeza kuwa hivi sasa kuna matapeli wa ardhi hasa viongozi wa vijiji ambao pindi wanapoombwa ardhi na wawekezaji, huwapimia ardhi hata ile iliyoko ndani ya pori tengefu kwa kisingizio kuwa hawajui mipaka ya vijiji vyao. Anasema kuwa viongozi kujifanya hawajui mipaka ni utapeli, hivyo pale itakapotokea watu waliouziwa maeneo na viongozi hao na kubomolewa, viongozi wa vijiji watawajibika kuwarudishia gharama zao kama si kuwatafutia ardhi mbadala kwenye maeneo ya vijiji vyao.


Mhe. Maige alisema kuwa kwa uharaka wa tatizo hilo la uvamizi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Bi. Monica Kagya ahakikishe kuwa tathimini inafanyika na fedha zinapatikana kwa ajili ya kuweka bikoni angalau kila baada ya mita 500 ili kutatua tatizo. Akielezea tatizo hilo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS alisema wakala wake uko mbioni kuajiri askari wa misitu watakaokuwa na jukumu la kuilinda misitu yote nchini ili kuondoa tatizo la uvamizi.


“Hivi sasa tuko katika mchakato wa kumalizia mpango kazi wa TFS na mara baada ya kumalizika tutatoa ajira kwa askari misitu ambao jukumu lao kuu litakuwa ni kuhakikisha misitu yetu haivamiwi. Hili litakuwa suluhisho la tatizo tulilonalo hivi sasa kwani muda wote misitu italindwa kama zinavyolindwa mashine za pesa,” alisema Bi. Kagya.

No comments:

Post a Comment