Sunday, January 8, 2012

KCB TANZANIA ILIPOICHIMBIA SHULE YA MSINGI MERU KISIMA CHA MIL 13/-


Mmoja wa wanafunzi Shule Msingi Meru iliyopo jijini Arusha Najma Jite, akiwaongoza wenzake kuimba kwaya wakati shule hiyo ilipokabidhiwa kisima cha maji kilichochimbwa kwa msaada na Benki ya KCB Tanzania kwa thamani ya shilingi Milioni 13/- hafla iliyofanyika hivi karibuni.
Wanafunzi wa Shule Msingi Meru iliyopo jijini Arusha, Najma Jite na Ally Fadhil wakichota maji baada ya kuzinduliwa kwa kisima kilichochimbwa kwa msaada na Benki ya KCB Tanzania kwa thamani ya shilingi Milioni 13/- wakati wa halfa iliyofanyika hivi karibuni.
Meneja wa KCB Tanzania tawi la Arusha, Bi Judith Lubuva akimfungulia maji mwanafunzi wa shule ya msingi Meru iliyopo jijini humo wakati wa hafla ya kukabidhiwa kisima cha maji kilichochimbwa kwa msaada na benki hiyo kwa thamani ya shilingi Milioni 13/-. Wanaoshudia ni baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo.
Meneja wa KCB Tanzania tawi la Arusha, Bi Judith Lubuva akimtishwa Samwel John ndoo ya maji ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Msingi Meru iliyopo jijini humo baada ya hafla ya kukabidhiwa kisima cha maji kilichochimbwa kwa msaada na benki hiyo kwa thamani ya shilingi Milioni 13/-. Wanaoshuhudia ni baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo.
Mwenyekiti wa shule ya Msingi Meru iliyopo jijini Arusha Abdul Kala akimkabidhi Meneja wa KCB Tanzania tawi la Arusha, Bi Judith Lubuva cheti cha shukurani baada ya kupokea kisima cha maji kilichochimbwa kwa msaada na benki hiyo kwa thamani ya shilingi Milioni 13/-. Kushoto ni Afisa Elimu wa jiji hilo Bw Omari Mkombole.
Afisa Elimu wa Jiji la Arusha Bw Omari Mkombole akifurahia jambo baada ya kuzindua rasmi kisima cha maji kilichochimbwa kwa msaada na Benki ya KCB Tanzania kwa thamani ya shilingi Milioni 13/-, hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu, Arusha
Benki ya KCB Tanzania imeendelea kuadhimisha wiki yake ya jamii hasa kwenye sekta ya elimu kwa kuichimbia kisima cha maji chenye thamani ya Milioni 13/- Shule ya Msingi Meru iliyopo kata ya Kati jijini Arusha.


Msaada huo ni kati ya shilingi Milioni 178.9/- zinazotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kusaidia jamii yenye uhitaji ikiwemo shule hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na ukosefu wa maji kwa kipindi kirefu hali iliyochangia wanafunzi kutohudhuria masomo kwa wakati wakitafuta maji mtoni. Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Meneja wa KCB Tanzania tawi la Arusha Judith Lubuva amesema lengo la benki yake ni kuhakikisha kiasi cha faida inachokipa kinarudi kwa jamii hususani kwenye sekta ya elimu, afya na mazingira ili kuchangia maendeleo.


Lubuva alisema kuwa, katika maeneo yenye uhaba wa maji wanafunzi ndio wanakuwa waathirika wakubwa kwani badala ya kuhudhuria masomo wamekuwa wakienda kutafuta maji kwa ajili ya familia zao na kuchangia kiwango cha mahudhurio darasani kushuka. “KCB Tanzania imeguswa baada ya kuona shule hii iliyopo katikati ya Jiji ikikosa maji hivyo walivyokuja kutuomba msaada wa maji tukaitikia mara ili kuwapatia wanafunzi huduma hii waliyokuwa wakiyafuata kwenye mto ulio pembezoni mwa shule hii,” alisema Lubuva.


Akizindua kisima hicho Afisa Elimu wa Jiji la Arusha Bw Omari Mkombole amesema kitendo kilichofanywa na benki hiyo ni cha kizalendo na kinaonesha nia ya kweli waliyonayo katika kumkomboia Mtanzania kutoka kwenye umasikini. Afisa Elimu hiyo aliongeza kuwa kabla ya uwepo kwa kisima hicho, maendelo ya wanafunzi Shule ya msingi Meru yalishuka kutokana na kupata maradhi yaliyotokana na matumizi ya maji ya mto.

“Tayari msaada huu wa kisima umeanza kuleta matunda kwa shule ya msingi Meru, maji yalipoanza kutumika yameinua kiwango cha walimu kutoa elimu kwani matokeo ya mwaka huu yanaonesha kwamba wanafunzi wote waliohitimu darasa la saba wamefaulu kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2012,” alisema Mkombole.


Akishukuru kwa msaada huo mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Samwel John amesema wanaishukuru KCB Tanzania kwa kuwapatia maji salama kwani sasa wataweza kuhudhuria masomo yao kwa wakati.
Hivi karibuni benki hiyo ilitumia kiasi cha Shilingi Milioni 11 kukarabati wodi ya wagonjwa mahututi ‘ICU’ na kununua vitanda vitatu katika hospitali rufaa ya KCMC iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment