Wednesday, January 25, 2012

TAARIFA KWA UMMA JUU YA MAAMUZI YA KAMATI KUU!

Taarifa ifuatayo inatolewa kwa umma kuhusu Maamuzi ya Mkutano wa Kawaida wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), uliofanyika kwa siku mbili tarehe 20 na 22 Januari 2012 katika Hoteli ya New Africa Jijini Dar es salaam.
Mkutano huo wa kawaida wa Kamati Kuu ulikuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo Uteuzi wa mgombea wa uwakilishi wa Jimbo la Uzini na kupitisha mkakati na bajeti ya uchaguzi husika; Taarifa ya Kamati Maalum ya Kamati kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na Taarifa ya Fedha (Mapato na Matumizi ya chama) kwa mwaka 2011.


Kuhusu Uchaguzi wa Uwakilishi katika Jimbo la Uzini: Katika kikao chake cha tarehe 20 Januari 2012, Kamati Kuu ilimteua Ali Mbarouk Mshimba kuwa mgombea wa uwakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Jimbo la Uzini kwa tiketi ya CHADEMA. Aidha, katika kikao chake cha tarehe 22 Januari 2012 Kamati Kuu ya chama imepokea na kujadili mkakati na bajeti ya uchaguzi wa Jimbo la Uzini. Kamati Kuu imeridhika na maandalizi ya awali ambayo chama kimeyafanya katika Jimbo husika na kuagiza sekretariati ya chama kufanya maandalizi zaidi kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni za uchaguzi husika.


Pia, kamati kuu imefanya mapitio ya bajeti na kuweka kikomo cha matumizi ya fedha katika uchaguzi tajwa ili kuhakikisha kwamba kampeni zinafanyika kwa ufanisi na kuendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa mikakati husika kwa kuzingatia mahitaji.Kuhusu Taarifa ya Kamati Maalum kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba: Kamati Kuu imepokea na kujadili taarifa ya Kamati Maalum kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 iliyoundwa na kamati kuu tarehe 20 Novemba 2011.

Pamoja na masuala mengine, Kamati Kuu ilitaarifiwa juu ya yaliyojiri katika mikutano kati ya Kamati Maalum ya CHADEMA na Rais Jakaya Kikwete na serikali tarehe 27 na 28 Novemba 2011 na tarehe 21 Januari 2012. Aidha kamati kuu ilijulishwa hatua ambazo serikali imefikia katika maandalizi ya kuifanyia marekebisho sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 katika Mkutano wa Sita wa Bunge unaotarajia kuanza tarehe 31 Januari 2012.

Kamati Kuu imeamua kwamba Kamati Maalum iendelee kufanya mawasiliano na mashauriano na Rais Kikwete na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 inafanyiwa marekebisho ya msingi kabla ya mchakato wa kukusanya maoni kwa mujibu wa sheria husika haujaanza.

Kamati Kuu imeendelea kusisitiza Azimio lake la kikao cha Novemba 20, 2011 kwamba “Ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo”.

Aidha, Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu hatua ambayo imefikiwa na chama katika kufanya mikutano ya ndani katika maeneo mbalimbali ya kuelimisha viongozi, wanachama na wananchi kuhusu upungufu wa sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 pamoja na kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha sheria husika.

Kamati Kuu ya chama imeamua kwamba CHADEMA kiendelee kutekeleza azimio la kikao cha Kamati Kuu cha Novemba 20, 2011 la kutoa “kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki”.


Kamati Kuu inaendelea kuwaagiza viongozi wote wa chama kama ilivyoelekezwa na Waraka wa Katibu Mkuu Namba 3 wa mwaka 2011, katika ngazi zote kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu kwa lengo la kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi.


Kuhusu Taarifa ya Fedha (Mapato na Matumizi ya chama) kwa mwaka 2011: Kamati kuu imetaarifiwa kuhusu vyanzo mbalimbali vya mapato ya chama kwa mwaka 2011. Aidha Kamati Kuu imetaarifiwa kuhusu matumizi ambayo yamefanywa na chama katika mwaka 2011 kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa chama 2011-2016 na Mpango Kazi wa mwaka 2011. Kamati Kuu imejulishwa matumizi yaliyofanywa katika utekelezaji wa mipango kwenye vipaumbele mbalimbali ikiwemo upelekaji wa ruzuku majimboni/wilayani/mkoani; ulipaji wa madeni ya uchaguzi mkuu wa 2010 na uwekezaji; uendeshaji wa makao makuu ya chama; utekelezaji wa operesheni za chama na mfuko wa uchaguzi mkuu 2015.

Kamati Kuu imepokea taarifa ya fedha kwa mwaka 2011 na kuagiza sekretariati ya chama kuandaa mkutano maalum kwa ajili ya kuendelea kujadili taarifa husika sanjari na Mpango Kazi wa Chama kwa mwaka 2012; taarifa zaidi kuhusu fedha na mipango itaelezwa baada ya mkutano huo.

Imetolewa tarehe 23 Januari 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi.

No comments:

Post a Comment