Sunday, July 31, 2011

MSAMA AUCTION MART YAKAMATA CD FEKI ZA MAMILIONI!

NA MWANDISHI WETU


KAMPUNI ya Msama Auction Mart,imefanikiwa kukamata CD feki zenye thamani ya mamilioni ya fedha,kutoka kwa wanyonyaji wa kazi za wasanii nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Alex Msama alisema kuwa hatua ya kukamata mzigo huo imekuja baada ya kuwekwa mitego mbalimbali ya kuwakamata wezi wa kazi hizo.
Msama alieleza kuwa mbali ya kukamata fedha hizo lakini pia wamefanikiwa kukamata fedha taslimu zaidi ya Sh. milioni 10 kutoka kwa wahalifu hao. Alieleza kuwa Kampuni yake kwa kushirikiana na jeshi la Polisi, imefanikiwa kuwatia nguvuni wanyonyaji na wasambazaji wakubwa wa kazi za wasanii zaidi ya nane,ambapo tayari baadhi yao wameshafikishwa Mahakamani.


Mbali ya kuwakamata wahusika lakini pia imefanikiwa kuukatama mitambo miwili mikubwa ya kudurufu CD yenye uwezo wa kuzalisha CD feki zaidi ya 300 ndani ya dakika 20. Alisema kuwa anaamini kazi ya kulitokomeza tatizo hilo linahitaji ushirikiano wa wadau wote wa muziki, lakini kutokana na kutopata ushirikiano atahakikisha anapambana.


“Ni kazi nzito kuifanya mwenyewe, lakini naamini nitafanikiwa tu,dawa yao nimeshaipata nitahakikisha nalipunguza kwa kiasi kikubwa au kulimaliza kabisa,”alisema.


Hata hivyo aliwalaumu wasanii na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA),kwa kukosa ushirikiano, ambapo alisema wadau hao wameziba plasta mdomoni kwa kutoliongelea kabisa suala hilo. Hata hivyo alieleza kuwa anaamini kutokana na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wanyonyaji na mitambo yao wangejitokeza kumuunga mkono, kitu ambacho hakijafanyika.

“Hakuna hata msanii mmoja anaeniunga mkono,zaidi ya ushirikiano wa dhati nanioupata kutoka ndani ya jeshi la Polisi, ila naamini nitafanikiwa,atakaeutambua mchango wangu atakuja kunishukuru ,”aliongeza.


Msama ameeleza kuwa amesambaza zaidi ya vijana 50,kushughulikia tatizo hilo, ambapo sasa wanakamata wanyonyaji wa aina zote za muziki bila kujali. Aliwataja baadhi ya wanyonyaji waliokwisha kamatwa kuwa ni Fred Jumbe,Martin Mkinga,Abdalah Kijemi,Abdalah Salum,Yahaya Salum,Razaro John,Amir Kasim,Faraj Amir,Rashid Juma na Mustafa Rashidi.

No comments:

Post a Comment