Wednesday, July 27, 2011

MRADI WA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA MAJI ZANZIBAR AWAMU YA PILI!

Tarehe 25 Julai, 2011, Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bwana Yukihide Katsuta, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati (MLHWE), Bwana Mwalim A. Mwalim, na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Dk. Mustafa Ali Garu, walitia saini Hati ya Makubaliano, ambayo ndio mkataba rasmi wa uzinduzi wa “Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Maji katika Mamlaka ya Maji, Zanzibar (Awamu ya pili)”.

Sekta ya maji ni moja kati ya sekta zinazopewa kipaumbele katika Mpango wa Japani wa Kuisaidia Tanzania (Japan’s Country Assistance Program). Katika Zanzibar, Japani imekuwa inasaidia kuboresha upatikanaji wa maji ya kudumu na ya uhakika sehemu za mijini kupitia miradi miwili: mradi wa ujenzi wa mabwawa ya maji na ujenzi wa mabomba ya usambazaji maji kupitia msaada wa ruzuku (grant aid) ambao ulimalizika Agosti, 2010. Aidha Japani imekuwa ikifadhili mradi wa kiufundi wa uanzishwaji wa huduma ya utoaji wa ankara za maji pamoja na uanzishwaji wa utaratibu wa malipo ya maji katika Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA). Mradi huu ulimalizika Desemba 2010.
 Hata hivyo imebainika kwamba uchakavu wa mitambo ya kusafirishia maji ndicho chanzo kikubwa kinachofanya kuwe na matatizo ya maji Zanzibar. Uchakavu huu unasababisha upotevu wa maji mengi (NRW) ikiwa ni pampja na uvujaji wa mabomba. Hivyo ni muhimu kwa ZAWA kupunguza upotevu huo kwa kuchukua hatua za kugundua uvujaji huo, utengenezaji wa mabomba na ukarabati wa mabomba. Kwa kufanya hivyo ZAWA itaweza kutoa huduma ya maji yenye uhakika.

Mradi uliotajwa hapo juu una madhumuni ya kuchangia katika uboreshaji wa huduma za maji zinazotolewa na ZAWA kwa kuimarisha uwezo wa kupunguza NRW pamoja na ukusanyaji wa ankara za malipo. Malipo hayo yatatumika barabara kutengeneza mitambo ya maji na hivyo kuwezesha watu wengi kupata maji yaliyo safi na salama.


Katika hotuba yake wakati wa shughuli ya kutia saini Hati ya Makubaliano hayo, Bwana Yukihide Katsuta, Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, alisema hivi: “Ni matumaini yangu kwamba mradi huu utatekelezwa vizuri chini ya uongozi thabiti wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati na Mamlaka ya Maji Zanzibar wakiwa na ari kubwa pamoja na msaada wa wataalamu wa JICA, ili watu wa Zanzibar waweze kufurahia matunda yake bila kuchelewa.”

No comments:

Post a Comment