Tuesday, June 7, 2011

JESHI LA POLISI MKOANI SINGIDA LAKAMATA KILO 400 ZA NYAMA YA NG'OMBE WANAODHANIWA KUIBIWA!

Jeshi la polisi mkoani Singida limekamata kilo 400 za nyama ya ng’ombe kumi, wanaodhaniwa kuibiwa Igunga mkoani Tabora siku ya Jumamosi iliyopita, wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni nne.

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Celina Kaluba amesema, nyama hizo zilikutwa kwenye maduka tofauti ya mfanyabiashara Ali Hamisi Irumba, yaliyopo eneo la soko kuu na Msufini, mjini Singida.


Kamanda Kaluba amesema, baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema, walifika kwenye moja ya duka la mtuhumiwa huyo, lakini alipowaona askari aliamua kukimbia.


Amesema baada ya hali hiyo, ilibidi askari wachukue nyama hizo hadi polisi na kuziuza kwa njia ya mnada, ambapo jumla ya Shilingi laki nne zilipatikana na kupelekwa Igunga kwa ajili ya ushahidi wa kesi iliyofunguliwa na mmiliki wake, Omari Ramadhani.


Bi.Kaluba amesema kuwa, kufuatia tukio hilo tayari wanamshikilia kijana mmoja aliyetajwa kwa jina la Nusura Hamisi na upelelezi zaidi unaendelea, ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment