NA KILEWO GWANDA
BINAFSI nimeguswa na namna vijana wanavyoshirikishwa kwenye mipango mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.Vijana wote kama ilivyo kwa wazee, wanawajibu wa kujenga uchumi wa taifa kutokana na rasilimali zilizopo.
Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MMM) yaliyoasisiwa miaka saba iliyopita na viongozi wa juu wa nchi 189 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), mjini New York, makao makuu ya umoja huo, yalileta matumaini makubwa kwa nchi nyingi duniani hasa nchi maskini.
Malengo haya yapo manane yakilenga kutokomeza umaskini, kutoa elimu ya msingi kwa watu wote, kuleta usawa wa jinsia, kupunguza vifo vya watoto wachanga, upatikanaji wa huduma bora za uzazi, kupambana na UKIMWI, malaria na magonjwa mengine; na la mwisho ambalo ni muhimu sana kwa nchi maskini ni kujenga na kuleta mshikamano wa kimaendeleo duniani.
Tukio la kuasisi Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MMM) ni la kihistoria kwani halijawahi kutokea duniani kwa sababu hapo mwanzo, mipango mingi sana iliyopitishwa haikuonyesha tumaini kwa sababu mbalimbali zikiwamo kutowashirikisha watu, mipango isiyo na muda, mipango mingine haikushirikisha jumuia za kimataifa, yaani kila nchi kutekeza mipango hiyo kivyake na mipango mingine kutotekelezeka.
Swali la kujiuliza ni kwamba, kwanini mpango huu umeleta matumaini makubwa kwa viongozi wa duniani? hapa kuna sababu nne zinazofanya mipiango hii kupewa heshima.
Mosi, mipango hiyo inayotekelezeka, pili, MMM ni mipango ya watu si viongozi, yenye muda maalumu wa utekelezaji, yaani miaka 15, tatu, inapimika, nne, ni mipango inayo lenga ushiriki wa dunia kwa pamoja katika kutimiza mipango hii, yaani kushirikiana na kusaidiana kwa nchi maskini na tajiri na pia kushirikisha asasi za kijamii.
Katika kutekeleza mpango huo, vijana wana wajibu mpana sana na kwa kujua hili, mwaka 2006 Asasi ya Vijana na Umoja wa Mataifa ya Tanzania –YUNA, kwa kushirikiana na asasi nyingine za Umoja wa Mataifa, ziliandaa kongamano la aina yake kutathmini malengo ya maendeleo ya milenia na ushiriki wa vijana, takriban nchi sita zilihudhuria; Kenya, Uganda, Tanzania, Afrika Kusini, Canada na Somalia.
Kongamano hili lilifanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, Nairobi Kenya.
Kongamano hili lilipewa jina la Eastern African Region Model United Nation-EARMUN (Baraza kivuli la Umoja wa Mataifa). Kongamano hili lilibeba kaulimbiu ya “Youth Actions towards MDGs”. Kaulimbiu hii, ilimpa kila kija changamoto kubwa na mpaka leo bado inawagusa.
Ukichunguza kwa makini utaona ni kauli ambayo inayomlenga mtu binafsi (yaani ni kauli inayo ISHI) na hili ni tukio ambalo lilishirikisha vijana wa kada mbalimbali, vijana walio kwenye asasi za kiraia, vijana walemavu, vijana wasomi, vijana wafanyakazi, vijana walio kwenye vyombo vya habari, vijana wa shule za msingi na sekondari na wengineo wengi.
Binafsi nilipata bahati ya kuwa moja kati ya waandaaji na washiriki kutoka Tanzania, pengine hii ni moja kati ya sababu kubwa inayo nifanya niandike makala hii. Ni haki na wajibu wetu kama washiriki wa warsha, makongamano na mafunzo mbalimbali kueleza umma tumejifunza nini na nini tunatakiwa kufanya!
Ikumbukwe kwamba asasi zozote zile ni mali ya umma, kwa hiyo rasilimali zinapotumika ni vizuri umma unufaike na kama viongozi au wanachama wa asasi ni wajibu wetu kuelezea umma mambo mbalimbali na mustakabali wa asasi husika.
Katika kuwasilisha hoja zangu kwenye makala hii, nimeanza na maswali mawili ya msingi, mosi, je, ni kweli vijana wameshirikishwa vya kutosha katika mpango huo? Pili, ni takriban miaka miwili tangu ripoti na takwimu za awali ya 2005 itoke, je, Tanzania itafikia malengo haya?
Takwimu zinaonyesha kuwa katika nchi nyingi za Afrika na duniani kwa ujumla, vijana (18-35), wanakaribia asilimia 60 au 70, kwa maana nyingine ni kwamba vijana ni wengi kuliko kundi lolote lile, yaani wazee, watoto na watu wazima ambao hawa wingi wao ni kati ya asilimia 40 na 30.
Cha kushangaza katika nchi nyingi za Afrika, kundi la vijana limesahaulika na mipango mingi ya serikali inawaacha vijana kwenye vichaka vizito kutokana na dhana potofu kuwa Wazee wana busara kuliko vijana, au kuamini maneno ya kejeli kuwa vijana ni taifa la kesho.
Hapa nchini, takwimu zinaonyesha kwamba vijana walio wengi hawajawahi kusikia na hawajui lolote kuhusu Malengo haya, pili, cha kushangaza zaidi hata hawa wachache waliosikia hawajui mipango hii kwa undani, tatu, hao wanaojua mipango hii kidogo hawajapewa fursa ya kuweza kutekeleza mipango hii!
Kama mipango hii ni kwa ajili ya wananchi ni vizuri wananchi (vijana) wakashirikishwa tangu mwanzo.
Maswali kama nini dhumuni la mpango huu? Kwa nini ni utekelezwe wakati huu? Kwa nini sisi ? kwa nini tushiriki? Upi ni ushiriki wetu? Upi ni mpaka wa ushiriki wetu? Rasilimali gani mpango utahitaji? Zitatoka wapi? Ni kiasi gani rasilimali hizi zitatumika? Tutashirikiana na nani? Kwa nini hawa? Haya ni maswali ya msingi kabisa kuyajua.
Kama jamii haitahamasishwa kutekeleza mpango huo, kuna hatari kuwa wataendeshwa na kauli ya ndiyo mzee! Pili, wananchi kwa sababu wanaendeshwa, mipango hii haitakuwa endelevu na hii ni mbaya na hapa ndipo mipango mingi sana inaposhindwa.
Ni vizuri wananchi wakamilikishwa mipango hii na Serikali na wadau wengine wasaidie pale panapotakiwa. Kwa mfano, utakuta wananchi wanajengewa shule, hospitali na masoko, lakini watu hawa hawavitumii vitu hivi na wakati mwigine kuviharibu.
Si ajabu kukuta wanakijiji wakikimbilia kilabuni kunywa pombe huku mkutano wa maendeleo ya kijiji ukiendelea. Hapa maana yake ni kwamba wananchi wanasema “pale hatuna chetu, mambo yote kilabuni!” Hapa maendeleo ni ndoto, kamwe hatuwezi kumwondolea mtu umaskini wake kama hatutamshirikisha!
Nilipata kusoma habari kuhusu kikundi cha vijana wa Malawi, kulikuwa na kikundi cha vijana wapatao watano wote walitoka kwenye familia maskini na wote walijua kusoma na kuandika tu! Walikuwa wakifanya biashara ya karanga! Inasemekana faida waliyokuwa wanapata ilikuwa ni ndogo mno kiasi cha kuwakatisha tamaa, lakini waliendelea!
Ilitokea siku wakapatiwa mafunzo na shirika la ujasiriamali la kigeni. Baada ya kupata mafunzo haya vijana hawa wakaweza kuandika miradi yao, kurekodi mapato na matumizi yao, kuainisha fursa mbalimbali pale kijijini kwao.
Baada ya muda wa miaka mitatu hivi kikundi kikabadilika na kuwa kampuni kubwa na kuweza kupata pato la zaidi ya kwacha 50,000,000! Kwa mwaka.Pia waliweza kuajiri vijana wenzao, kujenga ofisi nyingine kuanzisha miradi mingine na kushiriki kwa upana katika maendeleo ya eneo lao.
Hii inaonyesha wazi kuwa vijana wakipewa nafasi, muda, na rasilimali, wanaweza.
Katika kutekeleza MMM, vijana hawana budi kupewa mafunzo mbalimbali. Mfano jinsi ya kufikiria kwa mapana juu ya miradi na mbinu mbalimbali ya kuweza kujikwamua katika hali walizonazo, mafunzo juu ya kuandika miradi, iwe ya kibiashara, jinsi ya kutumia takwimu mbalimbali na kuangalia fursa zilizopo, jinsi ya kupata taarifa sahihi kwa wakati mwafaka, jinsi ya kufanya maamuzi, jinsi ya kuandika ripoti, mafunzo kama haya na mengineyo yaweza kuwasaidia sana vijana.
Serikali na wadau wengine wahakikishe wanaweka mipango hii kwa lugha rahisi ambayo hata yule anayejua kusoma na kuandika, ataelewa na kuweza kushiriki kikamilifu.
Tanzania imeweka MMM katika Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania, (MKUKUTA), mkakati huu umeandaliwa katika nguzo tatu, yaani ukuaji wa uchumi na upunguzaji wa umaskini, kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa jamii, utawala bora na uwajibikaji.
Mpaka sasa vijana walio wengi hawana ajira, walio wengi mlo wa siku ni tatizo, elimu ni ya ubaguzi, utawala umeendelea kuwabagua vijana, uhakika wa kupata maji safi na salama umekuwa wa shaka, na mengine.
Kwa kifupi viashirio vya MKUKUTA havijaonyesha kuwasaidia vijana tangu uasisiwe baada ya ule wa kwanza wa 2000. Moja ya sababu ya MKUKUTA kupata mafanikio hafifu ni ushiriki mdogo wa vijana na hapa ni sawa na kusema vijana wamekosa chombo cha kuwaunganisha na MKUKUTA!!
Kimsingi, limekosekana Baraza la Vijana la Taifa na Sera Imara ya Vijana! na bila ya chombo hiki, MKUKUTA hautawakuta vijana!
BAVITA kitakuwa chombo huru kitakachochukua uwezo wa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa masuala yote ya vijana kwa kushirikiana na taasisi za ndani na nje ya nchi, pia na chombo kitakachokuwa na uwezo wa kuchukua vijana wote wa CHADEMA, CUF, UDP, CCM, TADEA, NCCR, na ASIZE kama TYVA, YUNA, TDFY, TGEM TGNP, TANGO na vijana kutoka kada mbalimbali wasomi, wafanyakazi, wasio na kazi, wenye ulemavu. Pili, vijana tunataka sera mpya ya vijana ile ya mwaka 1996 imeisha, sera ambayo itatoa tafsiri kamili ya vijana si ya kubabaisha tu!
Wizara ya Kazi, Ajira, na Maendeleo ya Vijana, inafanya nini kama inashindwa kuanzisha BAVITA wakati mchakato ulishaanza? Wizara inaogopa vijana? Vijana hawawezi kuingia kwenye shirikisho kama wenzao wa Kenya na Uganda wana mabaraza.
Vijana wamekosa sauti. Mfano, Wizara imewafanya vijana mabubu. Tunapaswa kuuliza ni shilingi ngapi mawaziri, wabunge, rais wanatumia katika safari zisizo na tija? Wakati mwaka 2015 unakaribia, mpango huo uanze sasa kuwashirikisha vijana.
Kama una maoni plz unaweza kuchangia facebook..... www.theeastafrica.blogspot.com kwa uelewa!
No comments:
Post a Comment