Nape Nnauye akiwasha moto mjini Singida leo
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (pichani), amesema Mwenyekiti wa Chadema Freman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, ni mafisadi waliokubuhu ndani na nje ya chama hicho.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani ya mabasi mjini hapa, leo, Nape ameshusha tuhuma nzito kwamba licha ya kujinadi kila kona hapa nchini kuwa ni mpambanaji wa ufisadi, lakini amekiingiza chama chake katika mzigo mkubwa kwa kulazimisha kimlipe mshahara wa zaidi ya sh. Milioni 7 kwa mwezi.
Nape alisema, kudai kulipwa kiasi hicho cha mshahara licha kwamba ni ufisadi wa kuikandamiza Chadema pia ni ishara tosha ya unafiki alionao kwa kuwahadaa wananchi kwamba ana uchungu sana na fedha za umma wakati nafsi yake imejaa uroho na ufisadi mkubwa.
Alisema, wakati Dk. Slaa alipokuwa mbunge alikuwa akidai kwamba wabunge wanalipwa mshahara mkubwa wa sh. Milioni 6 kwa mwezi na kufanyia anasa wakati sh. Milioni 7 anazolipwa na Chadema ni nyingi zaidi zile za wabunge ambazo hata hivyo zinakatwa kodi wakati zake hazikatwi kodi.
Nape alisema, kama kweli Dk. Slaa ni muungwana na mpenda haki na mlinda mali ya umma aache mara moja kupokea mshahara huo na auombe radhi wanachama wa Chadema na Watanzania wote kuwa fedha anazolipwa zinatokana na kodi ya wananchi amabazo Chadema hupewa kama ruzuku.
Kuhusu Mbowe, Nape alisema, wakati naye akijitapa pia kuwa amtetea haki na mali za wanyonge Watanzania, naye bila aibu amekiuzia Chadema magari matatu 'machakavu' aina ya Fuso kwa milioni sh. 480. Nape alimshutumu Mbowe kwa kuuzia Chadema magari hayo huku akifahamu kuwa chama hicho ni taasisi ya umma na hivyo hakistahili kununua vifaa vilivyotumika tena kwa bei ghali kiasi hicho.
Alisema, inashangaza kuona kwamba Mbowe ameuza magari yaliyotumika kwa Tasisi ya umma ya Chama cha Chadema wakati yeye na viongozi wenzake wameibuka vinara hivi karibuni kupinga muswada wa serikali uliotaka masharti yalegezwe kwa baadhi ya taasisi ziruhusiwe kununua vifaa vilivyotumika usipelekwa bungeni.
Kwa muibu wa sheria ya sasa Taasisi za umma haziruhusiwa kununua vifaa chakavu, hatua ambayo imelifanya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) kushindwa kununua ndege walau iliyotumika ili iweze kujiendesha kibiashara kwa kuwa haliwezi kumusu kununua ndege mpya. Wakati huohuo, Nape amekibomoa Chadema mkoani Singida, zaidi ya wanachama 150 wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa Tawi la la Chadema Singida mjini Athumani Rajabu.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya watu, Nape alikabidhiwa kadi hizo na bendera za Chadema na mwenyekiti huyo ambaye alisema, ameamua yeye na wanachama wenzake kuhama Chadema kutokana na kuchoshwa na sera ya maandamano ya kila siku badala ya kuchochea maendeleo.
Kuhusu madai ya kuishiwa kasi ya kuwabana mafisadi ndani ya CCM, Nape alisisitiza kwamba hana msalie mtume kwa suala hilo, na kwamba msimamo ni ule ule wa kuwataka waondeke haraka. Katika Mkutano huo, Nape alifuatana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Chiligati, Katibu wa Uchumi na Fedha Taifa, Mwigulu Nchemba na Katibu wa Oganaizesheni Asha Juma Abdallah.
Viongozi hao wa Sekretarieti ya CCM, wapo mkoani Singida kwa ziara ya kikazi na kujitambulisha kwa wananchama wa CCM na wananchi kwa jumla ambapo wote kwa nyakati tofauti wamekuwa wakifafanua jinsi CCM ilivyodhamiria kuhakikisha CCM inakuwa chama cha wanachama na chenye maslahi kwa Watanzania wote.
Habari kwa hisani ya Bashiri Nkoromo
No comments:
Post a Comment